Kazi alizofanya Sheikh Ali bin Hemed


  1. Kwa ilimu yake alikubalika na kuadhimishwa Afrika Mashariki yote. Alipata kuwa Kadhi wa Tanga kuanzia mwaka 1339 Hijriah "1921" mpaka mwaka 1354 Hijriah "1935".Na aliendelea kufanya kazi nyingine za Serikali zilizokamatana na mas'ala ya dini.

  2. Alisomesha wanafunzi wengi wa mjini Tanga na waliokuja kutoka miji ya nje ya Tanga

  3. Amesafiri sana miji ya bara kwa ajili ya Tabligh ya dini na alikuwa ni mwenye sauti ya kusikiwa na kila mwenye kuhudhuria.

  4. Ametunga vitabu vingi vya lugha ya Kiswahili na harfu za kizungu.
    Katika vilivyotangaa zaidi ni kitabu chake cha Mirathi pamoja na mas'ala ya Wasiya na Hibba.
    Alikamilisha kukiandika kitabu hiki mwezi wa Septemba 1923 na kikapitiwa na kupasishwa na Sayid Ahmad bin Sumeyt na Sheikh Twahir bin Abubakar, Kadhi wa Zanzibar.

  5. Kitabu hiki cha Mirathi kilitafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na Bwana Philip Mitchell aliekuwa Bwana Shauri (Administrative Officer) wakati huo Tanganyika.
    Lakini pia kitabu hiki kilitumiwa sana katika Mahakama za Sheria, Afrika Mashariki, kila panapotokea haja ya kufutu mas'ala ya mirathi kwa mujibu wa sharia ya Kiislamu.

  6. Kitabu kingine kilichotangaa zadi ni "Taarifu Juu ya Tafsiri ya Wakadiani" alichokitowa mwaka 1954.
    Kitabu hiki kinabainisha uwongo wa Makadiani katika tafsiri yao ya Qur'ani waliyoitoa mwaka 1953

  7. Vile vile alianza kuandika tafsiri ya Qur'ani kwa lugha ya Kiswahili kwa kutumia harfu za Kiarabu.
    Mwenyiezi Mungu hakumjaalia umri wa kuweza kuikamilisha kazi hiyo. Alifariki baada ya kukamilisha tafsiri ya Suratul-An'aam.
    Tafsiri hiyo ambayo mwenyewe ameipa jina la "Al-Murshidul-Kariim Ilaa Tafsiyril-Qur'anil-Adhiim", inaandikwa tena lakini kwa kutumia harfu za kizungu ili itabiishwe na Waislam wapate kuisoma na kunufaika.
    Kazi hiyo ya kuandika tena kwa harfu za kizungu inafanywa na mwanawe Zuheri bin Ali bin Hemed.

1 comment:

  1. Assalaam,kwenye maulid ya watukuu na wajukuu wa Sheikh tupate video yake,itakua aula zaidi INSHAALLAH (SHARIFF)

    ReplyDelete